Exodus 40

Kuweka Wakfu Maskani Ya Mungu

1Kisha Bwana akamwambia Musa: 2 a“Simika Maskani ya Mungu, yaani Hema la Kukutania, katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza. 3 bWeka Sanduku la Ushuhuda ndani yake na ulifunike kwa pazia. Ingiza meza na kupanga vitu vyake juu yake. 4 cKisha ingiza kinara cha taa na uweke taa zake juu yake. 5 dWeka madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba mbele ya Sanduku la Ushuhuda kisha uweke pazia kwenye lango la Maskani ya Mungu.

6 e“Weka madhabahu ya sadaka za kuteketezwa mbele ya lango la Maskani ya Mungu, yaani Hema la Kukutania; 7 fweka sinia kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, na uweke maji ndani yake. 8 gFanyiza ua kuzunguka maskani na uweke pazia penye ingilio la ua.

9 h“Chukua mafuta ya upako, ipake Maskani ya Mungu pamoja na kila kitu kilichomo ndani yake; iweke wakfu pamoja na vitu vyote vilivyomo ndani mwake, nayo itakuwa takatifu. 10 iKisha yapake mafuta hayo madhabahu ya kuteketezea sadaka pamoja na vifaa vyake vyote; weka wakfu madhabahu nayo yatakuwa takatifu sana. 11Paka sinia mafuta pamoja na kishikilio chake na uviweke wakfu.

12 j“Mlete Haruni na wanawe kwenye ingilio la Hema la Kukutania na uwaoshe kwa maji. 13 kKisha mvike Haruni yale mavazi matakatifu, umtie mafuta na kumweka wakfu ili apate kunitumikia katikati ya ukuhani. 14 lWalete wanawe na uwavike makoti. 15 mKisha watie mafuta kama ulivyomtia baba yao, ili nao pia wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Kutiwa mafuta kwao kutakuwa kwa ajili ya ukuhani utakaoendelea kwa vizazi vyote vijavyo.” 16 nMusa akafanya kila kitu sawa kama vile Bwana alivyomwagiza.

17 oKwa hiyo Maskani ya Mungu ilisimikwa katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, katika mwaka wa pili. 18 pMusa alipoweka wakfu Maskani ya Mungu, aliweka vitako mahali pake, akasimamisha mihimili, akatia mataruma na kusimamisha nguzo. 19 qKisha akalitandaza hema juu ya Maskani ya Mungu na kuifunika hema, kama Bwana alivyomwagiza.

20 rAkachukua ule Ushuhuda na kuuweka ndani ya Sanduku la Agano, akaweka ile mipiko ya kubebea hilo Sanduku na kuweka kiti cha rehema juu yake. 21 sKisha Musa akalileta Sanduku ndani ya Maskani ya Mungu, akatundika pazia ili kulifunika Sanduku la Ushuhuda, kama Bwana alivyomwagiza.

22 tMusa akaweka meza ndani ya Hema la Kukutania, upande wa kaskazini ya Maskani ya Mungu nje ya pazia 23 una kupanga mikate juu yake mbele za Bwana, kama Bwana alivyomwagiza.

24 vAkaweka kinara cha taa ndani ya Hema la Kukutania mkabala na meza upande wa kusini mwa Maskani ya Mungu 25 wna kuziweka taa mbele za Bwana, kama Bwana alivyomwagiza.

26 xMusa akaweka madhabahu ya dhahabu ndani ya Hema la Kukutania mbele ya pazia 27 yna kufukiza uvumba wenye harufu nzuri, kama Bwana alivyomwagiza. 28 zKisha akaweka pazia kwenye ingilio la Maskani ya Mungu.

29 aaMusa akaweka madhabahu ya sadaka za kuteketezwa karibu na ingilio la Maskani ya Mungu, yaani Hema la Kukutania, na kutoa juu yake sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka kama Bwana alivyomwagiza.

30 abAkaweka sinia kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, akaweka maji ndani yake kwa ajili ya kunawia, 31 acNaye Musa, Haruni na wanawe wakayatumia kwa kunawia mikono na miguu yao. 32 adWakanawa kila walipoingia katika Hema la Kukutania au walipoikaribia madhabahu kama Bwana alivyomwagiza Musa.

33 aeKisha Musa akafanya ua kuizunguka Maskani ya Mungu na madhabahu, pia akaweka pazia kwenye ingilio la huo ua. Hivyo Musa akaikamilisha kazi.

Utukufu Wa Bwana

(Hesabu 9:15-23)

34 afNdipo wingu likafunika Hema la Kukutania, na utukufu wa Bwana ukaijaza Maskani ya Mungu. 35 agMusa hakuweza kuingia ndani ya Hema la Kukutania kwa sababu wingu lilikuwa limetua juu ya Hema, nao utukufu wa Bwana ukaijaza Maskani ya Mungu.

36 ahKatika safari yote ya Waisraeli, kila wakati wingu lilipoinuka kutoka juu ya Maskani ya Mungu, wangeondoka; 37lakini kama wingu halikuinuka, hawakuondoka, mpaka siku lilipoinuka. 38 aiKwa hiyo wingu la Bwana lilikuwa juu ya maskani mchana, na moto ulikuwa katika hilo wingu wakati wa usiku, machoni pa nyumba yote ya Israeli siku zote za safari zao.
Copyright information for SwhKC